PSSSF YAWATAKA WAANDISHI KUELIMISHA WANACHAMA KUHAKIKI TAARIFA ZA MICHANGO NA MAFAO KWA WAKATI

 Na

Paschazia Charles 

Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewataka waandishi wa habari kutumia majukwaa yao kuwaelimisha na kuwahamasisha wanachama kufanya uhakiki wa taarifa za michango na mafao yao kupitia mifumo ya kidijitali, ili kuhakikisha taarifa hizo zinakuwa sahihi na kuepusha changamoto wakati wa mchakato wa kudai mafao.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 18, 2026, mjini Shinyanga, wakati wa semina iliyoandaliwa na PSSSF kwa waandishi wa habari kutoka Klabu za Waandishi wa Habari za Shinyanga na Simiyu, pamoja na wanachama wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (Tanzania Bloggers Network – TBN).

Semina hiyo imewalenga kuwapa washiriki uelewa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na PSSSF, pamoja na namna wanavyoweza kutumia taaluma zao kufikisha elimu sahihi kwa jamii kuhusu hifadhi ya jamii.

Akizungumza katika semina hiyo, Msimamizi wa PSSSF Mkoa wa Simiyu, Salum Miraji, amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali ni sehemu ya maboresho yanayofanywa na mfuko huo katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama.

Amesema mifumo hiyo inamwezesha mwanachama kupata na kuhakiki taarifa zake akiwa mahali alipo, bila kuwa na ulazima wa kufika moja kwa moja katika ofisi za PSSSF.

Kwa mujibu wa Miraji, mwanachama anaweza kutumia mfumo huo kufuatilia taarifa mbalimbali, ikiwemo michango yake, na kubaini mapema iwapo kuna kasoro au taarifa zisizo sahihi zinazoweza kuleta changamoto wakati wa uchakataji wa mafao.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mfawidhi wa PSSSF Shinyanga, Sunday Rashid, amesema mfuko huo umeendelea kuchukua hatua za kuboresha maandalizi ya mafao kwa kuanza kushughulikia taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu miezi sita kabla ya kufikia tarehe yao rasmi ya kustaafu.

Amesema hatua hiyo inatoa nafasi ya kutosha kwa mfuko na mwanachama kufanya uhakiki wa taarifa na kushughulikia mapema changamoto zozote zinazoweza kujitokeza kabla ya mtumishi kustaafu.

Akifafanua kuhusu utaratibu huo, Sunday amesema PSSSF inaongozwa na kauli isemayo, “tunamlipa jana mtumishi wa kesho,” ikiwa na maana ya kuanza maandalizi ya mafao ya mtumishi mapema kabla ya kufikia tarehe yake rasmi ya kustaafu.

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru, amesema semina hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kwa waandishi wa habari na wanablogu kwa kuwa imewaongezea uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na PSSSF pamoja na masuala mbalimbali yanayowahusu wanachama na wastaafu.

Kakuru amesema elimu waliyoipata itawasaidia waandishi wa habari na wanablogu kuandaa na kusambaza taarifa zenye usahihi, huku wakitumia nafasi yao kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutumia huduma za PSSSF na kujikinga dhidi ya vitendo vya utapeli.

Amesema ushirikiano baina ya PSSSF, vyombo vya habari na wanablogu ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati na kuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya huduma za hifadhi ya jamii.

Naye Mratibu wa Tanzania Bloggers Network (TBN) Kanda ya Ziwa, Kadama Malunde, ameipongeza PSSSF kwa kuandaa semina hiyo, akisema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari na wanablogu kwa kuwa yanawaongezea maarifa kuhusu masuala wanayopaswa kuyafikisha kwa jamii.

Malunde amesema waandishi wa habari na wanablogu wana wajibu wa kuhakikisha taarifa wanazozifikisha kwa umma zinathibitishwa, zina usahihi na zinatokana na vyanzo vinavyoaminika, hasa katika kipindi ambacho taarifa za kidijitali zinaweza kusambaa kwa kasi.

“Semina kama hii ni muhimu kwa sababu inatupa nafasi ya kujifunza na kuongeza uelewa. Tukiwa waandishi na wanablogu, jukumu letu si kuchapisha taarifa tu, bali kuhakikisha taarifa tunazowafikishia wananchi ni sahihi, zimehakikiwa na zina manufaa kwa jamii,” amesema Malunde.

Semina hiyo imehitimishwa kwa msisitizo kwa waandishi wa habari na wanablogu kutumia majukwaa yao kutoa elimu kwa wanachama wa PSSSF kuhusu haki na wajibu wao, pamoja na namna ya kufuatilia taarifa zao za hifadhi ya jamii.

Aidha, waandishi wametakiwa kuwahamasisha wanachama kufanya uhakiki wa taarifa zao mapema kupitia mifumo ya kidijitali, badala ya kusubiri hadi wanapokaribia kustaafu au kufikia hatua ya kuhitaji mafao.







Download/Pakua/Install App ya APA HABARI Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia apahabarikadama@yahoo.com
Previous Post Next Post