Na Paschazia Charles
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), linaendelea na uchunguzi kufuatia madai ya kuwepo kwa mafuta yaliyochanganywa na maji katika kituo kimoja cha mafuta kilichopo mjini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa magari wanne waliodai kuwa magari yao yalipoteza nguvu mara baada ya kujaza mafuta katika kituo hicho.
Kwa mujibu wa walalamikaji, kuna uwezekano kuwa mafuta waliyonunua yalikuwa yamechanganywa na maji, hali iliyosababisha matatizo hayo ya kiufundi kwa magari yao.
Kamanda Magomi ameeleza kuwa uchunguzi unaendelea kwa kushirikisha wataalamu kutoka EWURA, ambao wana uwezo wa kupima na kubaini ubora wa mafuta, ili kupata ukweli wa madai hayo.
Aidha, amewataka wananchi waliotoa malalamiko kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, akisisitiza kuwa majibu rasmi na ya kitaalamu yatatolewa mara tu uchunguzi utakapokamilika.
