POLISI SHINYANGA WAWASHIKILIA WAWILI KWA KUZUA TAHARUKI 'UONGO WA KUPOTEZA SEHEMU ZA SIRI'

Na Paschazia Charles 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu wawili wakazi wa Wilaya ya Kahama kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo na kusababisha taharuki miongoni mwa wananchi, kufuatia madai yao ya kupoteza kimiujiza sehemu zao za siri.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, tukio la kwanza lilitokea Aprili 4, 2026 katika soko kuu la Kahama mjini, ambapo kijana mwenye umri wa miaka 22, Kisaka Elinihaki, alidai kupoteza sehemu zake za siri baada ya kuguswa bega la kushoto na Joseph Godfrey (36). Tukio hilo lilizua taharuki kubwa na kusababisha wananchi wenye hasira kujaribu kumshambulia Godfrey kabla ya kuokolewa na askari polisi.

Kamanda Magomi alieleza kuwa tukio la pili lilitokea Aprili 6, 2026 katika eneo la machimbo ya dhahabu Mwime, Kahama, ambapo mtu mwingine aitwaye Makoye James alitoa madai kama hayo dhidi ya Hamis Kumalija. Inadaiwa kuwa wawili hao walikuwa wakisafiri pamoja kwa pikipiki kabla ya tukio hilo, jambo lililosababisha mkusanyiko wa wananchi waliotaka kuchukua sheria mkononi, lakini polisi waliingilia kati na kudhibiti hali hiyo.

Hata hivyo, uchunguzi wa kitabibu uliofanywa umebaini kuwa madai ya watu hao hayakuwa ya kweli, kwani hakuna aliyekuwa na upungufu wowote katika sehemu zake za siri.

Kutokana na hali hiyo, polisi wamewakamata watuhumiwa hao kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na kusababisha taharuki katika jamii, huku hatua za kisheria zikiendelea dhidi yao.

Aidha, Kamanda Magomi ametoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa zisizo sahihi ambazo zinaweza kusababisha hofu na vurugu, na badala yake washirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama ili kulinda amani na utulivu wa nchi.




Download/Pakua/Install App ya APA HABARI Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia apahabarikadama@yahoo.com
Previous Post Next Post