TAKUKURU SHINYANGA YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 21 KUPITIA UFUATILIAJI WA MIRADI.

 Na

Paschazia Charles

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kurejesha zaidi ya shilingi milioni 21 baada ya kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026.

Kessy amesema fedha hizo zimeokolewa kupitia ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Awali na Msingi Tinde B iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, zaidi ya shilingi milioni 5.5 zimeokolewa kupitia ufuatiliaji wa mradi huo baada ya kubainika kuwa zaidi ya shilingi milioni 5.3 zilipaswa kulipwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama kodi ya zuio, huku shilingi 223,950 zikiwa ushuru wa huduma.

“Kupitia mapendekezo yaliyotolewa na ufuatiliaji uliofanywa, fedha zote zililipwa katika mamlaka husika,” amesema Kessy.


Aidha, amesema TAKUKURU imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia semina zinazohusisha taasisi za umma na binafsi pamoja na vyama vya msingi vya ushirika na masoko kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika jamii.


Pia ametoa rai kwa taasisi zote za umma kuhakikisha zinatoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya maadili na uwajibikaji.

Kwa upande mwingine, Kessy amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa hususan kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii.
"Wananchi wote niwaombe mkipata taarifa yeyote inayoashiria rushwa mtoe taarifa kupitia namba 113 bure kwani kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, hivyo niwaombe tutimize wajibu wetu" amesema Kessy.



Download/Pakua/Install App ya APA HABARI Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia apahabarikadama@yahoo.com
Previous Post Next Post